Jumatatu, 20 Oktoba 2014

MKUU WA WILAYA YA SAME AMEKIRI ONGEZEKO LA MIMBA ZA UTOTONI NA UKEKETAJI KUSHIKA KASI KATIKA WILAYA YAKE

MKUU wa Wilaya ya Same Mkoani Kilimanjaro, Herman Kapufi, amekiri kuwa Halmashauri ya Wilaya hiyo imezidiwa nguvu na wazazi ambao wanashirikiana na watuhumiwa wanaowapa mimba Wanafunzi ambao hawajamaliza masomo katika shule za Msingi na Sekondari Wilayani humo.

Kapufi ameyasema hayo wakati akiongea katika mazungumzo maalumu na waandishi wa habari, ambapo alidai jambo linaloisumbua Wilaya hiyo ni pamoja na watoto kukeketwa katika umri mdogo wakati Halmashauri ya Wilaya ikiwa inafanya juhudi za kuwakamata wanaoshiriki vitendo hivyo.

Hata hivyo alisema, katika kipindi cha mwaka jana takribani wanawake 37 wamekamatwa na Jeshi la Polisi katika eneo la Kavambughu wilayani humo wakiwa wanawakeketa watoto wachanga ambapo wamefikishwa mahakamani kujibu tuhuma dhidi yao (kesi bado inaendelea).

“Sheria za Nchi zinasema Msichana asiolewe akiwa na umri chini ya miaka kumi na nane awe anasoma au hasomi na kimsingi na wale wanaowakeketa wakiwa wadogo kabla hawajakomaa ili tusigundue bado tunaendelea kufanya uchunguzi ili kuwafikisha katika vyombo vya dola” alisema Kapufi

Takwimu zinaonyesha Wilaya ya Same imekuwa kinara wa kukeketa watoto wachanga na hivyo tatizo hilo kuwa sugu katika Wilaya hiyo.

Afisa Utawala wa Shirika lisilo la kiserikali linalojihusisha na maendeleo ya mwanawake Afya na Haki za Binadamu (LUDEF), Janeth Malibwi, alisema bado mila za ukeketaji katika Wilaya hiyo zinaendelea na kwamba kwa sasa wanakeketa watoto wachanga (pindi wanapozaliwa), jambo ambalo ni hatari kwa Afya zao



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni