Chama
cha Wanahabari Wanawake nchini - TAMWA kwa kushirikiana na Shirika la
Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Idadi ya Watu duniani (UNFPA) na
mashirika mengine yasiyo ya kiserikali wameungana katika kuadhimisha siku ya mtoto wakike Duniani yanayofanyika oktoba 10 kila mwaka kwa kufanya mjadala mpana juu ya kukomesha ndoa za utotoni hapa Tanzania.
Mjadala huo uliofanyika katika hoteli ya CMG-Motel mjini Tarime mkoani Mara na kufuatiwa na kilele chake kilichofanyika oktoba 11ni mwendelezo wa kampeni ya Kitaifa ya kutokomeza ndoa za utotoni ijulikanayo kama “Ndoa za umri mdogo, Ukanda Huru”
iliyozinduliwa mwaka huu ikiwa na lengo la kuboresha mienendo ya Taifa
kwa ajili ya kuhakikisha viongozi wanawajibika katika kukomesha ndoa
hizo kwa kuweka mikakati ili wasichana wapate haki zao.
Mwaka
2011, Baraza Kuu la Umoja wa Mataia lilipitisha maadhimio ya kuanzisha
Siku ya Mtoto wa Kike Duniani. Siku hiyo imetengwa kwa ajili ya
kuendeleza,kukuza haki na kutatua matatizo yanayowakumba wasichana.
Kauli mbiu mwaka huu ‘Kuwawezesha Wasichana: Kumaliza Mduara wa Ukatili’ ambayo inatoa
wito kwa wadau mbalimbali kutambua umuhimu wa kuwekeza, kuwawezesha na
kutokomeza aina zote za ukatili zinazowapata wasichana ikiwa ni pamoja
na ndoa za utotoni.
Ndoa
za utotoni ni suala linalohusu haki za binadamu; linakiuka haki za
binadamu na kuzuia maendeleo kwa wasichana na wanawake. Aidha katika
Tanzania pekee, wastani wasichana wawili kati ya watano wanaolewa kabla
ya kufikia umri wa miaka 18 wakati katika
bara la Afrika zaidi ya asilimia 42% ya watoto wa kike wanaolewa kabla
ya kufikia umri huo huku mamilioni wakiolewa wakiwa bado hawajafikia
umri wa kubalehe. Vilevile nchi 31 kati ya 41 duniani ambapo mwenendo wa
kuozesha watoto wa kike unakaribia asilimia 30% zimo Afrika.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni