Jumatano, 29 Oktoba 2014

WANAWAKE WAMEHAMASISHWA KUTUMIA FULSA ILIYOPO KATIKA SEKTA YA BAHARI

Wanawake wameaswa kutumia fursa iliyopo katika sekta ya bahari kwa kupata elimu na mafunzo ya sekta hiyo ambayo ni msingi wao katika kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia ukuaji sayansi na teknolojia inayoongezeka kwa kasi duniani.
 
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Usalama wa Mazingira Majini Tumpe Mwaijande kutoka Wizara ya Uchukuzi kwaniaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Shaaban Mwinjaka wakati wa ufunguzi wa mkutano wa mwaka wa Umoja wanawake walio katika Sekta ya masuala ya Bahari Mashariki na Kusini mwa Afrika (WOMESA) ulifanyika jana  Dar es salaam.
 

unnamed2
Mwenyekiti wa WOMASA kutoka Mauritius Bi. Meenaksi Bhirugnath Bhookun akitoa mada wakati wa ufunguzi wa mkutano huo
Akisoma hotuba kwa niaba ya Katibu Mkuu huyo, Mwaijande amewataka wajumbe wa mkutano huo (WOMESA), wawe tayari kujadili masuala yanayojenga na kukuza ushiriki wa wanawake katika sekta ya bahari katika nchi zao.
 
Katika mkutano huo wa siku nne ambao umeanza leo oktoba 28 na unatarajiwa kumalizika Oktoba 31 mwaka huu, mada mbalimbali zitajadiliwa ikiwemo mpango mkakati wa WOMESA kuhusu ushiriki wa wanawake katika masuala ya sekta ya bahari katika nchi wanachama. 
 
Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi kutoka Shirika la Kimataifa linaloshughulikia Mambo ya Bahari (IMO) Pamela Tansey amesema kuwa WOMESA imekuwa msatari wa mbele katika kumwendeleza mwanamke kwenye sekta ya bahari.
 
unnamed4
Picha ya pamoja ya wajumbe wa mkutano wa mwaka wa WOMASA mara baada ya ufunguzi wa mkutano huo.
Pamela amesisitiza kuwa wajumbe wa mkutano huo ni vema waelewe na kusimamia dira ya WOMESA ambayo lengo lake ni kuwawezesha wanawake kupata ajira katika sekta ya masuala ya bahari kwa njia ya kupta elimu na mafunzo katika kuendeleza taaluma yao juu ya masuala ya bahari.
 
Mkutano huo wa WOMESA unajumuisha wajumbe 52 kutoka nchi mbalimbali wanachama zikiwamo Ethiopia, Namibia, Komoro, Visiwa vya Shelisheli, Zambia, Mauritius na Kenya. 
 
Nchi nyingine ni Angola, Sudani, Lesotho, Uganda, Somalia, Eritrea, Botswana, Rwanda, Madagaska, Afrika Kusini, Msumbiji, Burundi, Malawi, Djibout, Zimbabwe na wenyeji Tanzania.
 
Mkatano huo wa siku nne unafanyika nchini chini ya ufadhili wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Taasisi ya Masuala ya Bahari Tanzania (DMI),   shirika la mfuko wa hifadhi ya jamii (NSSF) kwa kushirikiana na  Shirika la Kimataifa linaloshughulikia Mambo ya Bahari (IMO) na Shirika la Kimataifa la Maendeleo (UNDP).
 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni