Licha ya uwepo wa fikra tofauti juu ya maendeleo kwa wanawake mfadhili Melinda Gates, anaamini ukitaka kuisaidia Afrika kwanza anza na wanawake kwa kuwa ni ufunguo katika kukuza uchumi na maendeleo Afrika
Bi Melinda akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari mjini Paris hivi karibuni , kuhusu mradi wa kuchangisha fedha kwa ajili ya wanawake na wasichana alisema kuwawezesha wanawake ni miongoni mwa malengo yenye kipaumbele chenye nguvu katika taasisi ya Bill na Melinda Gates katika mkakati wa kuwasaidia watu katika nchi zinazoendelea kuwa huru katika nyanja ya afya, uzazi wa mpango na hali ngumu ya maamuzi kuhusu uchumi.
Hii ni kutokana na kuwa na ushahidi unaoonyesha wanawake barani Afrika , Asia na Amerika kusini wanauwezo mkubwa wa kuweka akiba ya fedha na kuirudisha katika matumizi ya familia kuliko wanaume wanavyofanya. Ambapo kuweka akiba huko kuna msaada kwa familia ya mwanamke na jamii kwa ujumla hali ambayo inashawishi kuwasaidia wanawake na wasichana katika maendeleo.
Kama kuna haja ya kukuza uchumi barani Afrika ni lazima uanze na wanawake licha ya kuwa mengi yanasemwa kuhusu mahitaji ya kuwawezesha wanawake ikiwemo ya kuzingatia katika kupunguza idadi ya uzazi na kuongeza jitihada za afya ya uzazi ambayo ni mkakati wa pili kati ya nane wa maendeleo ya milenia uliowekwa mwaka 2000 na jitihada kubwa zimefanywa kulisogeza hilo mbele.
Melinda amefafanua kuwa vifo vinavyotokana na uzazi vimepungua mara tatu kwa miaka 30 iliyopita na vifo vya watoto wachanga vimepungua kwa nusu ya ilivyokuwa kabla ya mpango huu. Makundi ya misaada yanafanya kazi kwa mpango mpya wa Milenia wenye lengo la kukuza usawa wa kijinsia na kuwawezesha wanawake ambako kutasaidia kupunguza umasikini na njaa.
Kwa mujibu wa ripoti ya kilimo na chakula ya Umoja wa mataifa ya mwaka 2010 -2011, kama wanawake watashirikishwa katika kilimo kwa nchi zinazoendelea kutaongeza mazao na hatimae kutasaidia kupunguza idadi ya watu wanaokosa chakula kwa asilimia 12 mpaka 17.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni